Search

TUVUNJE VIWANGO VYA UZURI VYA KIZUNGU NA KIKOLONI

Sote tumelazimika kuzoea viwango vya urembo vilivyopangwa na jamii, kwa hivyo ilibidi pia tuzoee kuhukumiwa kwa sababu ya rangi za ngozi zetu.


Watanzania wana rangi za ngozi zinazotofautiana, na tunafundishwa umuhimu wa rangi za ngozi zetu ndani ya jamii inayotuzunguka tangu utotoni. Tunakumbukumbu za maneno kama vile "mzuri" na "mbaya" yakifuatiwa na nyuso za wanawake wenye ngozi nyeupe zaidi na wenye ngozi nyeusi zaidi katika vitabu vyetu vya shule ya msingi, haswa vitabu vya somo la kiingereza.


picha inatoka: https://www.nccj.org/colorism-0

Wazungu waliokuja Afrika katika karne ya kumi na tisa walileta (pamoja na mambo mengine) dhana za upendeleo wa rangi. Wao ndio walioanza kuangalia rangi ya ngozi kama alama ya safu ya uongozi. Waafrika wenye ngozi nyeupe zaidi ndio ambao walifanana zaidi na wazungu, kwahiyo hao ndiyo waliohusishwa na ustaarabu na urembo - tofauti na wenzao wenye ngozi nyeusi zaidi. Wazungu waliona kwamba Waafrika wenye rangi nyeupe zaidi za ngozi ni bora na wanastahili kupewa upendeleo na hata vyeo. Hatusemi kwamba mizizi yote ya colorism imetokana na ukoloni wa Magharibi. Lakini pamoja na hili, mamlaka ya wakoloni ndiyo yaliyo tia chumvi na kutekeleza ubaguzi huu ambao wengi wameukubali kua hali ya maisha ya kawaida. Neno la Kiswahili "chotara", kwa mfano, linachukuliwa kama alama ya uzuri na utajiri kwa sababu machotara wamekubalika kama watu waliozaliwa kwa ukaribu na uzungu, na mara nyingi wanaitwa “Watanzania wa kigeni au uzunguni”.


Tumezoeshwa na kushinikizwa na jamii kuhusu uzuri wa mwanamke na rangi za ngozi zao. Wasichana wenye ngozi nyeusi zaidi wanataniwa na kauli kama "chausiku" au "mweusi kama mkaa". Neno "mweupe" limekubaliwa katika jamii ya Kitanzania kama pongezi badala ya kuangaliwa kama muenekano wa kawaida.


Colorism inaathiri kila mtu bila kujali jinsia, lakini inaathiri wanawake kwa namna tofauti. Mfumo dume ni moja ya sababu kuu inayopanga viwango vya kupima urembo katika jamii. Kwa namna hiyo, colorism, huathiri wanawake zaidi. Unyanyasaji wa kijinsia unafundisha wanawake kuweka jitihada katika kuwa na mvutio kwa ajili ya wanaume, na pia inafundisha wanaume kutafuta ngozi nyeupe zaidi kama kipimo cha uzuri wa mwanamke.


Unafiki huu unaathiri aina ya wanawake wanaooneshwa kwenye runinga, magazeti, mabango, matangazo na video za muziki. Unakuta wanawake weusi zaidi wanaonekana kwenye mabango ambayo yanatangaza dawa za kujichubua, na wanatumika kama picha ya kabla ya matumizi ya dawa hizo. Wanawake wa kitanzania ambao wana umaarufu na wanaofuatwa na watu wengi kwenye Instagram ni Wema Sepetu, Hamisa Mobetto, Jacqueline Wolper na Elizabeth Michael – wanawake wote hawa wana ngozi nyeupe. Hawa wanawake wanazingatiwa kama kipimo cha urembo ambacho wanawake wanapaswa kufuata. Vitu tunavyoviona na tunavyovichunguza kwenye mazingira yetu vinaathiri ni nini tunakiona ni kizuri. Kwahiyo, haishangazi kwamba kuna wanawake ambao wanachagua kujichubua ili wawe na mvutio kwa wanaume ambao wanatafuta wanawake weupe zaidi kuwa wapenzi wao.

picha zinatoka: (kuanzia kushoto hadi kulia) @hamisamobetto @ireneuwoya8 @wemasepetu @elizabethmichaelofficial kutoka instagram


Tunaishi kwenye jamii ambayo kuna faida na upendeleo wa watu wenye ngozi nyeupe. Wakati huo huo, kuna hasara za kuwa na ngozi nyeusi. Wanawake wenye ngozi nyeupe zaidi wanaonekana wakunjufu zaidi, pamoja na kuonekana kama ni wazuri zaidi na wana mvuto zaidi. Kwasababu hii, wanakuwa wanauwezekano mkubwa wa kuajiriwa, kutongozwa na kuposwa na pia kuaminiwa. Ila wanawake weusi zaidi wanakumbwa na ubaguzi, na wanaambiwa kwamba “wanaonekana kama wanaume” au “hawana mvuto”, au ni “wagomvi”.


Hii inatuleta kwenye swala labiashara ya uuzaji ya dawa za kujichubua, na kwamba hii ni sekta kubwa mno Tanzania. Mara nyingi, dawa za kujichubua zinatolewa kama dawa za kutibu chunusi na alama za chunisi kutokana na namna zinavyo fanya ngozi iwe nyeupe. Lakini lazima kuwe na dawa tofauti za chunusi ambazo hazitumii kemikali zinazoweza kusababisha saratani. Mara nyingi zaidi, unaona kwamba dawa za kujichubua zinatangazwa kama namna ya kufanya mtu awe “mzuri” zaidi. Hata hivyo, kuna aibu inayokuja kutokana na kuzitumia.


Wanawake ambao wanajikuta wakitumia dawa za kujichubua mara nyingi hawataki watu wajue; na ni kitu ambacho wanataka kukificha. Wanaitunza hii siri, kwa sababu hawataki kuaibika . Unakuta kwamba wanawake wenye ngozi nyeusi ambao wanakimbilia dawa za kujichubua wanachekwa na wanaaibishwa kwa sababu wanajaribu kuwa “weupe”. Kwahiyo, tunaishi kwenye jamii inayosukuma wanawake kutumia dawa za kujichubua, lakini hapo hapo pia, inawalaumu wakizitumia.


Picha imetoka: https://www.cosmeticconnection

Uzuri haupaswi kupimwa na kiwango cha weupe wa mtu. Kama tukilelewa kwenye jamii inayotufundisha kujipenda, nakupenda ngozi zetu bila kujaalisha ni rangi gani, tutakuwa na uwezekano mdogo zaidi wa kutafuta dawa za kujichubua ili tukidhi viwango vya kijinga na visivyo na msimamo. Lazima kuwe na utathminio mpya uangalizi wa kina dhidi ya vipimo vinavyo amua nani ni mtu mzuri” na mwenye “mvuto” katika jamii yetu. Ni lazima tufundishe vizazi vijayo kwamba uzuri hauna mipaka, bali ni viwango vinavyotengenezwa na jamii, na ni lazima tutafute namna za kuvivunja hivi viwango vibovu.


Kerin Shilla na Gloria Majule